Katibu Mteule wa Serikali ya Wanafunzi kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hussein Amri Aman, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu mwanafunzi Maria Godian Soko aliyefariki dunia kwa ajali kuwa alikuwa mjamzito na kwamba zinapaswa kupuuzwa.
Amri ameyasema hayo wakati akizungumza na www.eatv.tv, ambapo ameeleza kwamba marehemu Soko alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya pumu na ndiyo sababu kuu iliyomfanya awe anakimbizwa hospitali kwa ambulance.
Amesema, kutokana na ukaribu wake yeye na marehemu aliweza kumfahamu kuwa alikuwa akisumbuliwa na pumu kwa muda mrefu na mara nyngi humsababishia kupoteza fahamu.
"Marehemu Maria alikuwa na matatizo ya pumu ambayo yalimsababishia kifua kubana hadi kuzimia hivyo majira ya saa mbili kasoro tulifanya utaratibu wa kuita ambulance ya chuo na kumchukua hapa mabibo hostel kumpeleka hospitali ya chuo kwa matibabu zaidi"
Ameongeza "Wakati taratibu za kumpeleka hospitali ya chuo zinaendelea ndipo ajali mbaya ikatokea pale riverside, taarifa zinazoendelea kusambaa kwamba marehemu alikuwa mjamzito anaenda kujifungua sio za kweli".
Katika ajali hiyohadi sasa walioripotiwa kufariki ni wanafunzi wawili ambao ni Maria Godian Soko (Mwaka wa kwanza COSS) na Steven E Sango (CPE CoET mwaka wa pili) pamoja na dereva James
Mwanafunzi mwingine aliyekuwepo katika msafara huo ni Abishai Nkiko (Bsc Industrial Engineering mwaka wa 3 CoET) hali yake ni mbaya na anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya taifa ya muhimbili.
Maria Godian Soko ( B.A in psychology mwaka wa kwanza) amefariki jana usiku baada ya ambulance ya chuo kugongana na lori majira ya saa mbili maeneo ya riverside -Ubungo wakati alipokuwa akikimbizwa hospitali baada ya kubanwa na pumu hali iliyomfanya kupoteza fahamu.
Chanzo: EATV
Tags:
Habari