Sakata la Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutekeleza kanuni za maudhui, limewasilishwa bungeni na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea akitaka maelezo ya kina ya Serikali kwani inaminya uhuru wa habari.
Kubenea akitumia Kanuni ya 47 (1) (2) (3) leo bungeni Juni 12, 2018 akitaka kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili suala hilo.
“Kuanzia jana TCRA imesitisha usambazaji wa taarifa za social media, kwa tangazo hilo YouTube zote haziruhusiwi toka jana, Blog zote haziruhusiwi toka jana, website na redio zote ambazo ziko online haziruhusiwi toka jana,” amesema Kubenea na kuongeza:
“Kwa hiyo Mamlaka ya Mawasiliano wanasema mpaka Juni 15 mwaka huu, wale ambao watakuwa hawajalipia ada zao hawataruhusiwa. Mahakama Kuu kanda ya Mtwara ilisitisha hivyo nao wakazingatia agizo hilo la Mahakama.”
Kubenea amesema, “jana asubuhi, tangazo linatoka na watu hawajajiandaa, Bunge liahirishe shughuli zake za muda ili mjadala huu lijadiliwe na Serikali iweze kujibu suala hili, dunia imesimama hakuna taarifa zinatoka Tanzania kwenda kwingine na hata webstite zingine za serikali hazitoki nje.”
Akitoa maelezo ya kiti, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amesema, “hili la Kubenea sisi bungeni hatuwezi kuahirisha, waliofunga wana sababu zao na watakapokuwa tayari watafungua kama kawaida.”
Chanzo: Mwananchi
Tags:
Habari