Harusi ya Kiba Yawavuruga Bilnass,Christian Bella.

Harusi ya Kiba yawachanganya Bilnass, Christian Bella

Sherehe ya harusi ya msanii Ali Kiba, iliyofanyika jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena, imewachanganya watu mbalimbali wakiwemo wasanii Bilnas na Christian Bella.

MCL Digital iliyopata mwaliko katika sherehe hizo ilizungumza na wasanii mbalimbali ambao wamesema Kiba kawadhihirishia kuwa msanii ukiamua kuoa au kuolewa inawezekana.

Bilnas amesema kwake harusi hiyo imezidi kumchanganya zaidi baada ya kuona Kiba ameweza kuoa wazazi wake wote wakiwa bado hai, jambo ambalo ni la kumshukuru Mwenyezi Mungu.

“Kiukweli hii harusi wengi imetuchanganya na kutuamsha kuwa ukitaka kufanya jambo kama hili inawezekana tena inakuwa vizuri na wazazi wakalishuhudia kama alivyofanya mwenzetu Kiba.

“Amenitamanisha kiukweli na mimi niingie katika kundi la wanandoa, na ninaahidi nitafanya hivyo muda si mrefu,” amesema Bilnas mkali wa kibao cha Mazoea.

Kwa upande wake Christiana Bella, amesema harusi ya Kiba imempa fundisho naye sasa kuangalia namna ya kuanza kutoka kwenye maisha ya ‘ubachela’.

“Unajua si jambo dogo kwa msanii kijana kuamua kuoa akiwa katika umri mdogo, tunapitia vishawishi vingi ambavyo kama hutakuwa makini unaweza ukajikuta kila siku hutaki kuitwa mume wa mtu,” amesema.

Harusi hiyo ya Kiba imekuwa gumzo baada ya sherehe yake kufanyika mara mbili na kurushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam huku ikifuatiliwa na mamilioni ya watu. 

Post a Comment

Previous Post Next Post