Siku chache baada ya mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ kuangusha bonge la sherehe ya harusi katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar, wasanii wa Bongo Muvi wameibuka na kumtolea uvivu staa huyo.
NI KWA NINI?
Mastaa hao wa Bongo Muvi, wamedaiwa kumtolea uvivu AliKiba kwa kitendo chake cha kutowaalika katika sherehe yake hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita.
MSANII AVUJISHA MCHAPO
Mmoja wa wasanii wakubwa ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alivujisha mchapo kuwa, baada ya harusi ya Kiba kupita na kuona wasanii wa Bongo Muvi kama walitengwatengwa kwenye mnuso huo wa nguvu, ndipo walipoanika jamvini mjadala.
“Yaani harusi ilipopita, tukafanya tathimini na kuangalia idadi ya watu waliohudhuria. Tukagundua wengi ni mastaa wa Bongo Fleva, watangazaji na wadau wengine wasiohusiana na Bongo Muvi.
“Kwa kweli tukagundua jamaa ni mbaguzi. Hakuwa fair, alipaswa kuwaalika angalau mastaa wachache wa Bongo Muvi kuonesha ushirikiano, mbona sisi kwenye mambo yetu huwa tunaalika watu wote?” alihoji msanii huyo.
AMZUNGUMZIA ESHA
Kama hiyo haitoshi, msanii huyo alienda mbali zaidi kwa kusema, ameifanyia tathimini kwa kina zaidi harusi hiyo na kusema, hakuona Bongo Muvi aliyeenda katika harusi hiyo kwa kupewa mualiko.
“Wewe fuatilia, sanasana alienda Esha Buheti peke yake sababu kama unavyojua yule ana kaundugu fulani hivi na kina Kiba,” alisema.
WARAKA WANASWA
Wakati likiendelea kuichimba habari hiyo, Amani lilifanikiwa kuunasa waraka mzito ulioonesha masikitiko ya wasanii wa Bongo kwenda kwa AliKiba kwa kitendo chake cha kutowaalika.
Waraka huo ulisomeka hivi:
“Nimeshangazwa sana na AliKiba kwa alichowafanyia Bongo Movie, inashangaza kukosa kualikwa kwa wasanii angalau wachache wa Bongo Muvi, huu ni ubaguzi wa wazi.
“Sisi Bongo Muvi tumekuwa tukishiriki matukio mengi ya wasanii wa Bongo Fleva iwe harusi, misiba na hata maradhi, lakini kwa tukio la AliKiba tumejiuliza sana, wasanii kama Wema Sepetu, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Aunt Ezekiel, JB, Dk. Cheni, Ray, Richie, Gabo nk. ambao hata wachache chini ya hapo walifaa kualikwa.
“Tulimuona Esha Buheti lakini najua yule ni mwana familia kwa upande flani, sijajua ni kipi kimetokea kiasi cha kutokualikwa sisi, lakini kwenye video zao wamekuwa wakitualika ili tupendezeshe video zao, na hata kututaja ndani ya nyimbo zao,” ulisomeka waraka huo ambao unadaiwa kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na msanii Kulwa Kikumba ‘Dude.’
KIBA ATETEWA
Chanzo kingine kilichozungumza na Amani, kilieleza kuwa, Kiba alikuwa sawa kwani si lazima amualike kila mtu katika harusi yake kwani ni jambo lake binafsi na ukizingatia suala hilo lilitawaliwa na mambo ya timu za mjini.
“Unajua kuna watu hawakualikwa kwa sababu wapo timu Diamond (Nasibu Abdul), watu wa aina hiyo si rahisi kualikwa. Kwa hiyo waache kumlaumu Kiba,” kilisema chanzo hicho ambacho ni shabiki wa Kiba wa kindakindaki.
DUDE AJILIPUA
Amani lilimtafuta muigizaji Kulwa Kikuba ‘Dude’ ambaye alisema yeye pamoja na wenzake wa Bongo Muvi hawakufurahishwa na kitendo cha kutoalikwa.
“Kuhusu kuandika waraka mimi sina cha kukubali wala kukanusha ila tambua tu kuwa wasanii wengi wa Bongo Muvi hatukupenda kutengwa.
“Sisemi angenialika mimi au wasanii wote wa Bongo Muvi lakini hata baadhi tu kama kina Irene Uwoya, Wema Sepetu, Aunt Ezekiel, Steve Nyerere au JB basi angalau ingeonesha tuko pamoja,” alisema Dude.
Amani lilijaribu kuzungumza na baadhi ya wasanii ambao hawakuonekana kwenye harusi hiyo ambapo kila mmoja alitoa mawazo yake.
Aunt: Nisingependa kabisa kuongelea kuhusu hilo.
Wolper: Kwa kweli sikupewa mualiko lakini pia nilikuwa naumwa.
Steve Nyerere: Siwezi kulalamikia kutoalikwa kwenye harusi japo najua hayo mambo ya utimu yanaweza kuingia.
Amani lilimtafuta Alikiba bila mafanikio kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa lengo lilikuwa ni kutaka kusikia kwa upande wake anasemaje kuhusu madai ya kuwatenga wasanii wa Bongo Muvi kwenye sherehe ya harusi yake ambayo viwango vyake vilikuwa ni vya kimataifa.
Tags:
Burudani