DAR ES SALAAM: Ni giza nene! Madai yenye ujazo wa kutosha yanaendelea kutikisa kwamba memba wa Wasafi Classic Baby (WCB), Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ huenda akawa amejitoa kwenye lebo hiyo au pia yaweza kuwa vinginevyo, Gazeti la Ijumaa limeichimba kwa undani habari hii.
MADAI YA AWALI
Awali, madai ya bwa’mdogo huyo kutoka umakondeni Mtwara kujitoa yalianza kuibuka mara tu baada ya orodha ya wasanii watakaopafomu katika shoo ya ufunguzi wa Wasafi Festival iliyoanzia kwenye Viwanja vya Zimbihile, Muleba-Kagera. “Huyu dogo ameshajitoa, huwezi kumuona hata kwenye shoo hizi za Wasafi Festival, kama huamini subiria shoo ya ufunguzi utaniambia,” kilieleza chanzo kilicho karibu na mastaa hao.
Kama kilivyoeleza chanzo hicho makini, kweli Harmonize hakupafomu kwenye jukwaa hilo la ufunguzi Julai 19, mwaka huu, lakini hata hivyo, kabla hata ya shoo haijaanza, Rais wa WCB, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alikanusha madai hayo alipoulizwa sababu za Harmonize kutokuwepo kwenye orodha ya shoo hiyo.
“Harmonize hatutakuwa naye hapa, lakini kwenye shoo nyingine zinazokuja tutakuwa naye. “Unajua sasa hivi Wasafi ni kubwa, msanii anaweza kupata dili nje ya shoo yetu hatuwezi kumzuia. “Mfano hivi tunavyoongea Harmonize alikuwa na shoo Sudan tusingeweza kuwa naye, tutakuwa naye kwenye shoo nyingine kama vile Mwanza maana hatuwezi kusema lazima wasanii wote wa Wasafi tuwe nao, tutakuwa tunaenda tunabadilishabadilisha kulingana na nafasi zao,” alisema Diamond au Mondi.
TALE NAYE AKAZIA
Mbali na Diamond kuzungumza hivyo, meneja wa WCB, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ naye alinukuliwa akisema Harmonize hawatakuwa naye katika jukwaa la Muleba kwa sababu yupo nje ya nchi (Sudan) kwa ajili ya shoo na kufafanua kuwa waandaji wa shoo hiyo walitaka kumuongezea shoo nyingine nchini humo, lakini hata hivyo, hawakufikia muafaka.
“Kulitokea kama misunderstanding kati yetu na wale waandaji, awali walisema wangeweza kumuongezea shoo nyingine na ndiyo maana hata sisi hatukumweka kwenye orodha ya Muleba, lakini hata hivyo, baadaye wale waandaji tulishindwana, tukawa na sisi tumeshamkosa, tutakuwa naye kwenye shoo zinazokuja,” alisema Tale.
AIKOSA SHOO NYINGINE
Kwa kauli hiyo ya Tale, iliaminika huenda pengine Harmonize angepafomu kwenye shoo inayofuata ambayo ilikuwa ni ya Tabora (Julai 21, mwaka hu), lakini nayo hakuwepo.
KESHO YAKE AKAIBUKA NA ISHU YAKE
Wakati mashabiki wakiamini kwamba huenda mara baada ya kurejea nchini Harmonize angekwenda moja kwa moja kuungana na wenzake, lakini haikuwa hivyo.
Badala yake alirejea nchini na siku moja baada tu ya ile shoo ya Tabora kufanyika, Harmonize aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar na kufungukia ‘project’ yake mpya na msanii mkongwe kwenye Bongo Fleva, Abubakar Katwila ‘Q Chillah’. Alipoulizwa siku hiyo kuhusu kutoonekana kwenye jukwaa la Wasafi, alijibu kwa kifupi kuwa ataungana nao hivi karibuni na mashabiki watamuona kwenye shoo hizo za Wasafi Festival zinazoendelea.
IJUMAA LAMFUNGIA KAZI
Kutokana na uzito wa madai hayo na majibu ya Harmonize, Tale na Mondi kuonesha bado kuna giza nene kwenye ishu hiyo, Gazeti la Ijumaa liliamua kwenda mbele zaidi kwa kutinga katika makao Makuu ya Wasafi, Mbezi Kwa Zena jijini Dar ili kujiridhisha kama jamaa huyo yupo pamoja na memba wenzake au la.
WALINZI HAWAJAMUONA MWEZI…
Hata hivyo, licha ya kukutana na ugumu wa kuwapata wahusika, Ijumaa lilizungumza na walinzi wa eneo hilo ambao walisema hawajamuona Harmonize ofisini hapo kwa takriban mwezi mmoja nyuma. Walinzi hao walisema wanavyosikiasikia ni kwamba Harmonize ana ofisi yake mpya maeneo ya Sinza-Kijiweni jijini Dar, lakini wakasema hawana uhakika kama amehamia huko jumla au la.
“Hatujajua kama amehamia huko jumla au la, lakini tunasikia anakuwa huko sana labda mumfuatilie huko,” alisema mmoja wa walinzi waliokuwepo, lakini hakutaka kujitambulisha jina. Ijumaa lilijaribu kuisaka ofisi hiyo, lakini hadi tunakwenda mitamboni, halikufanikiwa kuifikia. Jitihada zinaendelea!
CHANZO CHAZIDI KUKAZIA
Chanzo kilichozungumza awali na Ijumaa kilizidi kusisitiza kuwa, kuna uwezekano mkubwa Harmonize akaamua kujikita zaidi katika kuanzisha lebo yake ya Konde Gang na ndiyo maana akamzawadia gari Q Chillah ambaye tayari wamefanya kazi tatu za pamoja. “Ameanza na Chillah, inaonekana kabisa ataongeza wasanii wake wengine kwani anaamini anaweza kusimama mwenyewe kwa sasa, ninyi sikilizieni kama mtamuona huko Mwanza,” kilisema chanzo.
KITENDAWILI KUTEGULIWA KESHO
Kwa kauli aliyoitoa Mondi Muleba kuwa Harmonize atapafomu katika jukwaa la Wasafi Festival jijini Mwanza, kitendawili hicho kitateguliwa kesho pale ambapo shoo hiyo itachukua nafasi katika Ukumbi wa Rock City Mall.
Tags:
arts & entertainment